(C) Global Voices
This story was originally published by Global Voices and is unaltered.
. . . . . . . . . .



Kwa nini Kiswahili hakijawa lugha inayounganisha Afrika? [1]

['Njeri Wangari']

Date: 2022-10-14 09:06:33+00:00

JULAI 7 ilikuwa siku kubwa kwa Afrika iliposherehekea kwa mara ya kwanza Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Wananchi kote Kenya, Tanzania, Zanzibar, Afrika Kusini, na ulimwenguni waliadhimisha siku kwa kusherehekea barabarani na mitandaoni kwa kutumia heshtegi #KiswahiliDay2022 na #KiswahiliDay. Hii ilikuwa siku ya kwanza rasmi tangu UNESCO ilipotenga Julai 7 kama siku ya lugha ya Kiswahili kuadhimishwa kote duniani mnamo November 2021.

Tume ya Kiswahili Afrika (KAKAMA), shirika lisilo la kiserikali ambalo linahimiza na kuratibu ustawi wa Kiswahili, lilipatiwa fursa ya kwanza fursa ya kwanza kupanga matukio ya kuadhimisha siku kote Afrika Mashariki. Waandalizi waliandaa hafla katika makao makuu ya KAKAMA yaliyovutia wanachama kadha wa mataifa shirika katika Jumuia ya Afrika Mashariki.

Wakenya pia walitembea katika barabara za Jiji Kuu la Nairobi kuadhimisha sherehe hizo kwenye msafara ulioongozwa na Waziri wa Utalii nchini na Mkuu wa Kamati Simamizi ya Kitaifa ya Siku ya Kiswahili Duniani 2022, Najib Balala.

Nchini Uganda, baraza la mawaziri liliidhinisha hoja kutumia Kiswahili kama lugha rasmi kufuatia uamuzi wa Februari mwaka uliopita wakati wa kongamano la 21 la Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo waliafikiana kutumia Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili kama lugha rasmi za jumuia hiyo. Baraza la mawaziri Uganda pia lilipendekeza shule za msingi na sekondari kufundisha Kiswahili darasani. EAC ni jumuia ya kieneo inayojumuisha nchi saba wanachama: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mataifa ya Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, makao yake makuu yakiwa Arusha, Tanzania. Kiswahili ni lugha rasmi katika nchi zote sita washirika wa Uganda.

Nchini Tanzania, serikali ilitangaza mipango ya kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili na imetenga ekari 100 maeneo ya Pwani ya Bagamoyo kwa ujenzi wa mradi huo.

Mtandaoni, video iliyomjumuisha kiongozi wa upinzani Afrika Kusini Julius Malema akizungumzia umuhimu wa kufundisha na kujifunza Kiswahili kama lugha ya kimataifa na kuhimiza Waafrika kukikumbatia Kiswahili kama lugha ya Afrika, iliibua hisia mseto kutoka kwa wananchi kote Afrika na kufufua mdahalo ambao unaendelea miongoni mwa wajuzi wa lugha na watetezi wa tamaduni: Kiswahili kinaweza kuwa lugha kuu ya Afrika?

The South African and EFF leader, Julius Malema calling upon all #African countries to embrace #Swahili as their national #Language.#Kiswahili is spoken by over 200 million people.#SwahiliDay #KiswahiliDay #WorldKiswahiliDay #KiswahiliLanguageDay pic.twitter.com/vbWceGFmD8

— Wako Joel (@WakoJoel) July 7, 2022

[END]
---
[1] Url: https://sw.globalvoices.org/2022/10/kwa-nini-kiswahili-hakijawa-lugha-inayounganisha-afrika/

Published and (C) by Global Voices
Content appears here under this condition or license: https://globalvoices.org/about/global-voices-attribution-policy/.

via Magical.Fish Gopher News Feeds:
gopher://magical.fish/1/feeds/news/globalvoices/